Daktari ateuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Jordan Valley
dakika 3 za kusoma
Bodi ya Jordan Valley Community Health Center yamteua Dkt. Matt Stinson kuwa Rais na Afisa Mtendaji Mkuu ajaye
SPRINGFIELD, MO - Bodi ya Wakurugenzi ya Jordan Valley Community Health Center (JVCHC) inafuraha kutangaza uteuzi wa Matthew Stinson, M.D., kuwa Rais na Afisa Mkuu Mtendaji ajaye wa shirika. Kwa sasa Dkt. Stinson ni Makamu wa Rais Mtendaji wa Huduma za Afya ya Msingi na Afya ya Kitabia wa Jordan Valley na amekuwa sehemu ya timu ya wafanyakazi kwa miaka 17. Ataanza rasmi majukumu ya Rais na Afisa Mkuu Mtendaji wa JVCHC tarehe 1 Juni 2024.
Bodi ilianza mchakato wa kutafuta na kuajiri kiongozi mwishoni mwa 2023 baada ya Rais na Afisa Mkuu Mtendaji wa sasa, K. Brooks Miller, kutangaza nia yake ya kustaafu kutoka kwenye nafasi hiyo mwaka 2024. Miller alisaidia kuanzisha Kliniki ya Afya Inayokidhi Vigezo vya Serikali ya Shirikisho zaidi ya miongo 2 iliyopita. Chini ya uongozi wake, Jordan Valley imepanuka na kujumuisha huduma za matibabu, meno, macho na huduma nyingine katika maeneo kadhaa ya Springfield pamoja na kliniki za Hollister, Lebanon, Marshfield na Republic. Kwa sasa JVCHC inaajiri zaidi ya watu 730 katika eneo hili.
"Tulipoanza mchakato wa kutafuta kiongozi, wajumbe wa bodi walichukua muda kuomba ushauri kutoka kwa wenzao ambao wamepitia mabadiliko kama haya kutokana na kustaafu kwa kiongozi mwanzilishi," alisema Mwenyekiti wa Bodi Mike Schnake. "Juhudi hizo za makusudi ziliunda mchakato na mpango wa kuajiri unaoendana na nia yetu ya kuwa na mabadiliko madhubuti na yasiyo na vikwazo ya uongozi, yanayohifadhi utamaduni wetu, kutanguliza huduma kwa wagonjwa wetu na kuiweka Jordan Valley katika nafasi ya kuendelea kufanikiwa. Tuna imani kamili katika uwezo wa Dkt. Stinson wa kutimiza dhamira na maono hayo."
Dkt. Stinson alijiunga na JVCHC mwaka 2007 kama daktari wa familia na mwaka 2010 alichukua jukumu la Mkurugenzi wa Matibabu. Mwaka 2014, alijiunga na timu ya watendaji wa Jordan Valley, akichukua jukumu la kimkakati zaidi katika upanuzi wa programu kama vile Express Care, huduma jumuishi za afya ya kitabia na huduma za upimaji wa macho.
Dkt. Stinson ni mhitimu wa Southwest Baptist University na St. Louis University School of Medicine. Ni rais wa zamani wa Greene County Medical Society na amewahi kuwa mjumbe wa bodi za mashirika ya eneo hili yasiyo ya faida kama vile Child Advocacy Center. Katika ngazi ya jimbo, hivi karibuni alihudumu katika Kamati ya Uidhinishaji wa Awali ya MO HealthNet. Dkt. Stinson anatetea uasili wa watoto na ana shauku ya kuwahudumia watoto walio katika mazingira hatarishi. Yeye na mkewe Chandra wamekuwa katika ndoa kwa miaka 28 na wana watoto 11, 5 wa kuwazaa na 6 wa kuasili. Nje ya kazi, Dkt. Stinson huwa na shughuli nyingi na hushiriki kikamilifu katika maisha ya watoto wao 7 ambao kwa sasa wanaishi nyumbani.
"Ninapokea fursa hii kwa unyenyekevu na shukrani," alisema Dkt. Stinson. "Itakuwa heshima kuongoza timu hii ya wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu ambao wote wana dhamira ya dhati iliyokita mizizi katika kutimiza lengo la Jordan Valley - kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kuzitoa kwa ubora na huruma. Nguvu yetu inatokana na kuendelea kuzingatia ubunifu ili kuwahudumia wagonjwa wetu kwa kiwango cha juu zaidi. Kazi hiyo inajumuisha miradi inayoendelea sasa kama vile mabadiliko yetu yajayo ya kuanza kutumia mfumo wa Epic wa rekodi za afya za kielektroniki (EHR) wenye tovuti iliyopanuliwa ya wagonjwa, kuongeza rasilimali zetu za mafunzo kwa wanafunzi wa uanagenzi wa usaidizi wa matibabu na meno, na kuanzisha Programu yetu ya Huduma Jumuishi kwa Wazee (PACE)."
"Mfano wa uongozi wa kuwatumikia wengine wa Brooks Miller utakuwa nguzo ya kudumu ya msingi wa Jordan Valley," alisema Mwenyekiti wa Bodi Schnake. "Daima atakuwa mtetezi mkuu wa kuboresha upatikanaji wa huduma na kupanua mfumo huu wa huduma unaomweka mgonjwa katikati. Tunamshukuru sana yeye na timu nzima ya Jordan Valley kwa kujitolea kwao bila kuyumba kwa wote tunaowahudumia."